TANGAZA NASI KWA BEI NAFUU

Alhamisi, 16 Mei 2013

Redd’s Miss Tanzania yashika kasi


Hashim Lundenga.
Na Mwandishi wetu
KINYANG’ANYIRO cha Redd’s Miss Tanzania kinazidi kushika kasi, huku tayari warembo 11 wakiwa wamepatikana kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino, Hashim Lundenga alisema, wamejivunia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa warembo hao, huku sehemu nyingine nazo zikisaka washindi wao.
 
Lundenga alisema, mpaka sasa vituo 10 kati ya 80 vinavyotakiwa kutoa warembo watakaoendelea katika hatua inayofuata ya Redd’s Miss Tanzania, vimeshapata warembo wao.
 
Alivitaja vituo ambavyo vimepata warembo wao kuwa ni, Dar Indian Ocean, Arusha City Centre, Mbeya City Centre, Ilemela, Nyamagana, Tarime, Serengeti, Mbulu, Hai na Kahama
 
“Huu ni mwaka wa 20 tangu tuanze mashindano yetu, nichukue fursa hii  kuwashukuru wadhamini wetu wote waliojitokeza kudhamini mashindano yetu kuanzia ngazi ya chini kabisa ya vitongoji.
 
“Mwaka huu tutakuwa na mikoa 24 inayofanya mashindano, kanda zipo 11, vyuo vya elimu ya juu vinavyoshiriki ni 17, wilaya 18 na vituo vya Mkoa wa Dar es Salaam 11, vyote kwa pamoja vinafanya idadi ya vituo zaidi ya 80,” alisema Lundenga.
 
Alisema wiki hii kutakuwa na mashindano ya kusaka warembo ndani ya Moshi Mjini, Kibaha, Chuo cha Ustawi wa Jamii, Ubungo na Mzima.
 
“Nawashukuru wazazi na walezi ambao wamewaruhusu watoto wao kushiriki katika sehemu mbalimbali, niwashukuru pia wadhamini mbalimbali waliojitokeza kudhamini mashindano yetu katika ngazi mbalimbali,” alisema Lundenga.
 
Meneja wa kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Victoria Kimaro alisema, wamedhamiria kuhakikisha Redd’s Miss Tanzania inakuwa mbali zaidi.
 
“Nawaomba tuendelee kukiunga mkono kinywaji hiki ili nacho kiweze kupata nguvu ya kuwaletea burudani hii ya urembo kwa muda mwingi zaidi,” alisema Victoria.
 
Taji la Redd’s Miss Tanzania kwa sasa linashikiliwa na Brigette Alfred, aliyetokea kitongoji cha Sinza, huku likiwa linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na TBL.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni